Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan cha jijini Dar es Salaam Profesa Msaidizi Peter Kajoro, amesema hayo leo wakati wa kongamano la Hisabati kwa nchi za Afrika Mashariki, kongamano lililoandaliwa na Tume ya Kimataifa ya Maelekezo na Ufundishaji wa somo la hisabati na kuhudhuriwa na wataalamu zaidi ya mia moja.
Profesa Kajoro amesema mbinu hiyo imetumiwa na mataifa mengi yaliyofanikiwa katika ufundishaji na ufaulu wa somo la hisabati na kufafanua kuwa somo hilo lina uhusiano mkubwa na utamaduni wa eneo husika na kwamba kitendo cha somo hilo kufundishwa kwa lugha na tamaduni za kigeni kimechangia kupunguza hamasa na ufaulu miongoni mwa wanafunzi.
Wakati huo huo, serikali ya Tanzania imesema haina uhakika wa kiwango cha huduma na ufanisi wa kazi kinachoonyeshwa na watumishi wa umma, hususani wale wa idara zinazohudumia wananchi moja kwa moja, huku ikiwataka wananchi kutoa mrejesho serikalini kuhusu ubora wa huduma wanazopata kutoka kwa taasisi na idara husika.
Naibu Katibu wa Idara ya Utumishi serikalini Bi. Neema Tawale amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari, alipokuwa anazungumzia tathmini ya Tume ya Utumishi wa Umma, juu ya uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za masuala ya ajira katika utumishi wa umma.
Bi. Tawale amesema katika kuongeza kiwango cha ufanisi wa watumishi wa umma, Tume imekuwa ikishirikiana na sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma, ili kuhakikisha kuwa udahili wa watumishi unazingatia elimu, sifa na vigezo vya ajira na kwamba katika baadhi ya nyakati, tume imewachukulia hatua za kinidhamu maofisa na watendaji wakuu ambao wamebainika kukiuka taratibu na sheria za utumishi wa umma.