Kila Mtanzania nchini atakuwa na uwezo wa kupata simu ya kisasa na yenye uwezo mkubwa (smart phone) kwa bei ya chini kabisa katika miaka mitano ijayo kuanzia mwaka 2020 kwa mujibu wa mipango ya kampuni mpya ya simu inayojiandaa kuingia katika soko la simu la Tanzania.
Aidha, Kampuni ya Viettel ya Vietnam imemwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumatatu, Oktoba 27, mwaka huu, 2014 kuwa itateremsha kwa kiasi kikubwa bei ya simu za kawaida na smart phone, ili kuwezesha kila Mtanzania kuwa na simu.
Kampuni hiyo pia imemwambia Rais Kikwete kuwa itasambaza mawasiliano ya internet kwa kila kijiji nchini na kuwa kwa taasisi za umma kama vile shule, hospitali, vituo vya polisi zitapatiwa huduma hiyo bila malipo yoyote.
Rais Kikwete ameambiwa habari hiyo njema kwa Watanzania na Mwenyekiti wa Kampuni ya Simu ya Viettel wakati alipotembelea makao makuu ya Kampuni hiyo mjini Hanoi kwenye siku yake ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Kiserikali katika Vietnam.
Mwenyekiti wa Kampuni hiyo ya umma ambayo inamilikiwa na Jeshi la Vietnam, Bwana Nguyen Manh Hung amemwambia Rais Kikwete kuwa Viettel inakusudia kumwezesha kila Mtanzania kumiliki smart phone kwa kupunguza bei ya simu hiyo na pia kupunguza bei ya huduma muhimu kama vile ile ya internet.
Bwana Hung amesema kuwa Kampuni yake inapanga kupunguza bei ya simu za kawaida hadi kufikia dola za Marekani 15, sawa na shilingi 25,000 na punguza ile bei ya smart phone hadi kufikia dola za Marekani 40, sawa na shilingi 65,000. S asa hivi, bei ya simu hizo ni kubwa mara nyingi ya kisai hicho kinachokusudiwa.
“Tunataka kuifanya bei ya kununua smart phone kuwa mara 10 chini ya bei ya kununua kompyuta. Tunasukudia pia kupunguza bei ya matumizi ya simu kuwa dola moja tu ya Marekani, sawa na shilingi 1,600, kwa watu wa kawaida kwa mwezi na kwa wale ambao wanatumia simu kwa huduma nyingi zaidi watalipa dola za Merakani 50, sawa na shilingi 78,000, kwa mwezi,” amesema Bwana Hung.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa Kampuni yake itawekeza kiasi cha dola za Marekani bilioni moja katika huduma za simu na huduma nyingine katika Tanzania na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili nyuma ya Peru kupata mfumo wa simu wa kisasa zaidi miongoni mwa nchi ambako Kampuni hiyo ina shughuli zake.
Amesema kuwa ndani ya miaka mitatu tokea Kampuni hiyo kuanza shughuli zake katika Tanzania, kiasi cha vijiji 4,000 ambavyo kwa sasa havina mawasiliano vitapatiwa huduma hiyo katika awamu ya kwanza.
“Katika awamu ya pili, kiasi chavituo 150 vya polisi, hospitali za umma 150, ofisi za Shirika la Posta kiasi cha 65 nchini vitapatiwa huduma ya mawasiliamo yakiwemo ya internet bure katika mwaka wa kwanza wa Kampuni hiyo kuanza shughuli zake. Tutatoa pia huduma ya internet na mfumo wa teknolojia ya mawasiliano bure kwa shule 450 za umma katika wilaya 150 ambazo tayari zina umeme, huduma ambazo pia zitatolewa katika mwaka wa kwanza wa Kampuni hiyo kuanza kazi,” amesema.
Bwana Hung amesema kuwa Kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 1989 iliingia katika shughuli za simu mwaka 2000 na kuanza shughuli za simu za mkononi mwaka 2004.
Mwaka jana, mapato ya kampuni hiyo yalikuwa ni dola za Marekani bilioni 9.1 na kati ya hizo kampuni hiyo ilikuwa imepata faida ya karibu dola za Marekani bilioni moja.