Waziri wa ujenzi uchukuzi na mawasiliano nchini Tanzania Profesa Makame Mbarawa amemsimamisha kazi mkurugenzi wa fedha wa shirika la Ndege Tanzania ATCL Steven Kasubi kwa kuhusika katika upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 700 kupitia kwa wakala wa uuzaji ticketi wa nchini Commoro.
Waziri Mbawala amebainisha hayo hii leo wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari na kumtaja wakala Salama World Traveler kuwa ndiye mhusika mkuu wa upoteaji wa fedha hizo kwa kushirikiana na mkurugenzi wa fedha wa shirika la Air Tanzania.
Amesema mkurugenzi huyo alikiuka utaratibu uliowekwa na serikali kuwa wanaruhusiwa kutoa tiketi kwa mawakala zisizozidi thamani ya shilingi milioni 15 na mteja atapewa tena tiketi baada ya kurejesha pesa yote lakini Salama World Travel aliruhusiwa kuuza tiketi za zaidi ya shilingi milioni 100 mara tano mfululizo bila ya kurejesha fedha za mauzo.
Aidha shirika hilo limetakiwa kufanya ukaguzi kwa mawakala wote wanaouza tiketi za ndege za kampuni ya Air Tanzania na yeyote atakayebainika kusababisha ubadhirifu wa fedha ya serikali hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa juu yao.








