Friday , 24th Aug , 2018

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, LAAC, imemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, Revocatus Kuuli, kuchagua kati ya kuendelea na nafasi yake ama awasiliane na mamlaka husika aweze kuachia ngazi.

Kushoto ni Mwenyekiti wa kamati ya LAAC Mh. Vedasto Ngombale na kulia ni Makamu Mwenyekiti Abdallah Chikota.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mh. Vedasto Ngombale, ametoa maagizo hayo katika moja ya vikao vya kamati za Bunge vinavyoendelea jijini Dodoma kwa kile alichokieleza kuwa Mkurugenzi huyo ameshindwa kuwahudumia wananchi kutokana na kutokuwepo ofisini muda mwingi na badala yake kuwaachia wasaidizi wake.

''Mkurugenzi huyo ameshindwa kutimiza wajibu wake wa kusimamia Halmashauri na kuwahudumia wananchi na iwapo hawezi anapaswa kujiuzulu nafasi hiyo kwa kuwasiliana na mamlaka zilizomteua na hii ni kwa manufaa ya wananchi wa Igunga'', amesema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Chikota, ametoa maagizo kwa uongozi wa Halmashauri ya Bukoba Mjini  kwa kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Limbe Maurice, kuchukua hatua stahiki kwa viongozi ambao hawatekelezi majukumu yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Limbe Maurice, amesema atahakikisha anatekeleza maagizo yote waliyopewa na kamati hiyo ndani ya muda husika. Kamati za Bunge zinaendelea na vikao katika kumbi mbalimbali za Bunge jijini Dodoma kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge Septemba 4 mwaka huu.