Maafisa wakagua jengo lililoanguka Nairobi nchini Kenya
Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya limesema idadi ya vifo imefika watu 12 na wengine 134 waliojeruhiwa waliokolewa kutoka kwenye vifusi, wengine wakiokolewa na raia na wafanyakazi wa uokozi waliotumia mikono kufanya kazi hiyo.
Waokoaji jana walisema waliweza kusikia sauti za watu watano ndani ya vifusi vya jengo hilo. Rais Uhuru Kenyatta alizuru eneo la tukio hilo kujionea maafa yaliyotokana na kuporomoka kwa jengo hilo. Mwaka jana, Kenyatta aliamuru kufanywa ukaguzi wa usalama wa majengo yote nchini Kenya.
Mamlaka ya Taifa ya Ujenzi Kenya ilibaini kuwa kuwa asilimia 58 ya majengo katika Jiji Nairobi ambalo ndio Mji Mkuu wa Kenya hayafai mtu kuishi ndani.
Maafisa wa Mamlaka ya Ujenzi wamesema baadhi ya wakandarasi wa ujenzi wanakiuka sheria ili kukamilisha haraka miradi ya ujenzi kutokana na kuongezeka kwa biashara ya nyumba.