Saturday , 3rd Dec , 2016

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inahitaji ushirikiano mkubwa na wafanyabiashara, hivyo haitakubaliana na mtumishi yeyote wa umma atakayefanya urasimu kwa lengo la kukwamisha uboreshaji wa sekta binafsi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda mkoani Arusha kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha (AICC), akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani humo.

Ziara hiyo inayolenga kuangalia utelelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM, utendaji wa serikali, kusikiliza na kujionea kero zinazowakabili wananchi wa mkoa huo, na kushirikiana na viongozi wa mkoa ili kuweza kuzipatia suluhisho.

“Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kukuza uchumi wa nchi yetu, pia mapambano dhidi ya rushwa yanayofanyika ndani ya serikali na nje yanalenga kuleta maboresho makubwa katika sekta binafsi ,” alisema.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa serikali inawataka watendaji wake wote watumie lugha nzuri na rafiki katika kutoa huduma kwa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla, na haitamvumilia mtumishi yeyote atakayefanya urasimu ili mfanyabiashara atoe rushwa.

“Hatuwezi kuzungumzia maendeleo katika sekta za maji, madini na viwanda bila ya kutaja wafanyabiashara kwa sababu hata viwanda wao ndiyo wamiliki, wafanyabiashara wameondoa vijana wengi waliokuwa wanakaa vijiweni na kujadili mambo yasiyokuwa na tija na kuwaajiri kwenye viwanda vyao,” alisema Mh. Majaliwa.