Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini. Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Tarehe 6 Julai 2016. Pamoja na kutambua bei kikomo za bidhaa mbalimbali za petroli kwa nchi nzima, ni muhimu kuzingatia yafuatayo:-
Bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote yaani Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepanda ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 1 Juni 2016.
Kwa Mwezi Julai 2016, bei za rejareja zimepanda kama ifuatavyo; Petroli Sh 23/lita sawa na asilimia 1.26, Dizeli Sh88/lita sawa na asilimia 5.36 na Mafuta ya Taa Sh 80/lita, sawa na asilimia 5.01, sawia.
Aidha, kwa kulinganisha na toleo la mwezi uliopita bei za jumla nazo pia zimepanda kama ifuatavyo; Petroli Sh 23.46/lita sawa na asilimia 1.34, Dizeli Sh 87.54/lita sawa na asilimia 5.74 na Mafuta ya Taa Sh80.48lita sawa na asilimia 5.37, sawia. Kwa kiasi kikubwa, mabadiliko haya ya bei za mafuta katika soko letu la ndani yametokana na kuendelea kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia.




