Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Alhaj Dkt Ali Mohmaed Shein amewaongoza mamia ya wananchi katika kisomo maalum cha hitma ya kumuenzi Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume na mashujaa wengine wa Zanzibar.
Kisomo hicho kilichofanyika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui nakuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali ya mapinduzi Zanzibar na serikali ya muungano wa Tanzania akiwemo makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilali , makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharrif Hamad na wa pili balozi Seif ali Iddi na viongozi wengine wa vyama vya siasa na dini akiwemo mufti mkuu wa Zanzibar Shekh Saleh Kabbi.
Wengine ni mama Mwanamwema Shein ambaye amewaongoza wanawake wakiwemo familia ya Karume iliyokuwa na mjane mama Fatma Karume ambapo hitma hiyo imeongozwa na ustadhi Sharrif Muhidini.
Baada ya hitma hiyo Sheikh wa mkoa Dar es salaam Alhad Mussa Salum amemsifu marehemu karume kwa utendaji wake wa kuwatumikia wananchi huku akiwakumbusha wananchi kuwa kifo ni hakichagui mtu na lazima watu wajiandae.
Baada ya kisomo hicho viongozi hao wakuu wameshirki katika uwekaji wa mashada ya maua katika kaburi la marehemu karume ambapo mbali ya Dkt Shein viongozi wengine waliofuata kuweka mashada hayo ni makamu wa Rais Dkt Mohamed Gharib Bilal kwa niaba ya Rais Kikwete akifuatiwa na mnadhimu mkuu wa jeshi la wananchi na vikosi vya ulinzi luteni jenerali Samuel Ndomba balozi mdogo wa china Xie Yualing kwa niaba ya mabalozi, na kufuata mzee Hamid Ameir kwa kuwakilisha wazee na wana mpinduzi huku balozi Ali Karume akiwakilisha familia ya marehemu Karume.
Baada ya uwekaji huo wa mashada ya maua viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali walipata fursa ya kusoma dua na kumuombea marehmu Abeid Karume na mashujaa wote huku Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume akitoa salamu zake kwa wananchi.
Wazanzibari na watanzania wote wanakumbuka tarehe ya April Saba miaka 43 iliyopita mwaka 1972 ndio siku ambayo Rais wa kwanza na muasisi wa mapinduzi hayati Abeid Amani Karume aliuwawa.