Thursday , 10th Dec , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa zaidi ya elfu mbili huku wafungwa 117 wakitarajiwa kuachiwa huru ikiwa ni sehemu ya kadhimisha sherehe za Desemba 9.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Magereza Jenerali wa Magereza John Minja imesema msamaha huo utawahusu wagonjwa wa UKIMWI, kifua kikuu na saratani, wafungwa wazee, wafungwa wa kike walioingia gerezani na ujauzito pamoja na wale wanaoingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa msahama huo hautawahusu waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa, waliohukumiwa kifungo cha maisha pamoja na makosa ya mauaji.

Pia msamaha huo hautawahusu wanaotumikia adhabu ya kujihusisha na usafirishaji na utumiaji wa madawa ya kulevya, unyang'anyi wa kutumia silaha , wafungwa wa makosa ya shambulio la aibu, Jinai, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.

Imeongeza kuwa msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kufungwa kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na shule za sekondari ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka 18.