Thursday , 11th Feb , 2016

Watu 11 wamefariki dunia wakiwemo madereva wawili na mtoto mmoja na wengine 29 kujeruhiwa baada ya basi la abiria la Simba Mtoto kupata ajali kwa kugongana na lori Mkoani Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Mihayo Msikhela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Pangamlima Barabara ya Tanga-Segera wilayani Muheza na kuongeza kuwa kati ya majeruhi hao wawili hali zao ni mbaya.

Akielezea Chanzo cha Ajali hiyo Kamanda Msikhlea amesema kuwa ni uzembe wa dereva wa lori ambaye inasemekana alisinzia na kuhama upande wake na kuhamia upande mwingine wa barabara na kusababisha magari hayo kugongana uso kwa uso.

Kamanda Msikhela amesema kati ya watu waliofariki dunia sita wamekwisha tambuliwa akiwemo mtoto wa miaka miwili huku akiongeza kati ya vifo hivyo kumi na moja wanaume ni nane na wanawake ni watatu akiwemo na mtoto huyo huku akibainisha pia waliojeruhiwa wanaume ni 19 na wanawake ni 9.

Aidha Kamanda amesema kuwa majeruhi 24 wote wanaendelea vizuri na wanaendelea kupatia matibabu katika hospitali ya Muheza na wawili waliojeruhiwa vibaya mmoja yupo cha upasuaji kwa uangalizi zaidi.