Wednesday , 6th May , 2015

Mamlaka ya Uendelezaji wa zao la korosho nchini Tanzania - CIDTF imeanza mchakato wa ujenzi wa viwanda vitatu vya kubangua na kuongeza thamani ya zao la korosho inayolimwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Zao la Korosho, Bw. Athuman Nkinde (kushoto), akikabidhi mche bora wa zao la korosho kwa mmoja wa wadau wa zao hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mamlaka hiyo Bw. Athuman Nkinde, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati mamlaka hiyo iliposaini makubaliano ya usanifu, ujenzi na mpango wa biashara, utakaotumika katika ujenzi na biashara ya korosho zitakazobanguliwa katika viwanda hivyo.

Katika makubaliano hayo, Chuo Kikuu cha Ardhi kitahusika katika usanifu na usimamizi wa ujenzi wa viwanda hivyo wakati Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itahusika na ubunifu wa mpango wa biashara ambao mamlaka hiyo itautumia katika uendeshaji wa viwanda hivyo.

Nkinde ametaja maeneo ambako viwanda hivyo vitajengwa kuwa ni katika wilaya za Tunduru mkoani Ruvuma, Mkuranga mkoa wa Pwani na Mtwara Mjini katika eneo la Mangamba mkoani Mtwara.

Akifafanua kuhusu namna viwanda hivyo vitakavyofanya kazi, Bw. Nkinde amesema kila kiwanda kitaanza na uzalishaji wa tani kumi za korosho kwa mwaka, huku vikitumika pia katika uongezaji thamani pamoja na ufungishaji wa korosho zinazozalishwa na vikundi vodogo vidogo vya akina mama katika maeneo husika.

Nkinde amesema uzalishaji wa viwanda hivyo utakuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka, huku mipango ya ujenzi wa viwanda katika maeneo mengine yanayolimwa korosho kwa wingi ukiendelea.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Bw. Mudhihiri Mudhihiri amesema hatua ya ujenzi wa viwanda hiyo ni ukombozi kwa wakulima ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawana mahala wangeuza na kupata soko zuri la korosho zao.

Kwa mujibu wa Mudhihiri, kukosekana kwa soko zuri la korosho kunatokana na ubinafsishaji usio na tija wa vilivyokuwa viwanda vya kubangulia korosho ambapo waliouziwa viwanda hivyo wamevigeuza kuwa maghala ya kuhifadhi bidhaa za dukani huku wengine wakiyageuza kuwa karakana za kutengenezea magari.

Mudhihiri ameweka wazi kuwa hatua ya ujenzi wa viwanda hivyo utazalisha uhasama kutoka kwa wafanyabiashara wanaosafirisha korosho nje ya nchi na ambao wasingependa kuona korosho za Tanzania zinabanguliwa na kuongezwa thamani hapa hapa nchini.

Ameongeza kuwa juhudi zinazofanywa na mamlaka ya uendelezaji wa zao la korosho zina mwelekeo mzuri na kwamba ana imani mopaka kufikia mwakani viwanda hivyo vitaanza kufanya kazi na kuwa suluhisho la bei na soko zuri kwa wakulima.