Wednesday , 17th Oct , 2018

Baada ya kuvuja kwa sauti inayodaiwa kuwa ya wabunge wa CHADEMA, Antony Komu wa Jimbo la Moshi Vijijini na Saed Kubenea wa Ubungo wakijadili namna ya kumuondoa katika nafasi yake meya wa manispaa ya Ubungo Boniface Jacob kwa maelezo kuwa ni mpambe wa mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe

Mbunge wa Moshi Vijijini (CHADEMA), Anthony Komu (kulia) na Saed Kubenea Mbunge wa Ubungo.

Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Vincent Mashinji amesema chama hicho bado hakijachukua hatua zozote za kuwahoji wabunge hao.

Hapo awali zilisambaa taarifa mitandaoni kuwa chama hicho kimewataka wabunge hao wajieleze kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu na kamati kuu ya chama hicho kwa kujihusisha na usaliti dhidi ya chama, hata hivyo Dkt. Mashinji ameieleza www.eatv.tv, kuwa wamesikiliza sauti za wabunge hao mitandaoni tu na hakuna hatua ambazo wamechukua dhidi yao mpaka sasa.

"Hatujaandika barua kwa mbunge yeyote na tumesikia kupitia mitandao, sikuwepo ofisini ngoja tuone kwakuwa ndio nimerudi ngoja tuone litashughulikiwa vipi", amesema Mashinji.

Chama hicho mapema jana kupitia Mkurugenzi wa  Itifaki, Mawasiliano na mambo ya Nje, John Mrema kuwa kilitoa taarifa kwa Umma kuwa leo kamati kuu ya CHADEMA inakutaka kwa dharura kujadili masuala mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya chama hicho.

Kikao hiki kitakuwa na ajenda kuu ya kujadili na kuazimia kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya chama, tutatoa taarifa rasmi juu ya maazimio ya kikao hiki kitakapomalizika", ilisema taarifa hiyo.

Mpaka sasa wabunge saba wa CHADEMA wamejiuzulu na kujiunga na CCM kwa kile walichoeleza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli na wengine wakielekeza mashambulizi kwa Mbowe na chama hicho.