Monday , 10th Nov , 2014

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemtaka mkuu wa jeshi la polisi nchini kuwachukulia hatua kali za kisheria askari wake wawili wanaotumiwa kuwaua raia.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Freeman Mbowe amemtaka mkuu wa jeshi la polisi nchini kuwachukulia hatua kali za kisheria askari wake wawili wanaotumiwa kuwaua raia, kuwatishia silaha pamoja na kuwabambikizia kesi za mauaji baadhi ya wakazi wa tarafa ya Bulyankulu wilaya ya kaliua mkoani Tabora.

Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Mh. Freeman Mbowe amewasili kwa helikopita akiwa katika ziara ya Operesheni Delete CCM na mara tu baada ya kupokelewa na wenyeji wake anakabidhiwa risala iliyojaa malalamiko mwanzo mwisho.

Akihutubia mkutano wa hadhara makao ya wilaya ya kaliua kabla ya kuelekea wilayani Sikonge, mwenyekiti huyo wa CHADEMA taifa amemtaka katibu mkuu wa chama cha mapinduzi Abdulrahaman Kinana kuacha kuwachezea shere wananchi kwa kuanza kuwalaumu baadhi ya viongozi wa serikali huku akijua fika kuwa chama chake ndicho kinachoongoza serikali.

Na kisha Mh. Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akatoa tahadhari kwa watanzania.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Tabora Francis Msuka pamoja na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA mkoa wa Tabora Sada Hoka Kadezi wamekemea vitendo vya unyanyasaji na uonevu vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya maafisa watendaji wa vijiji dhidi ya wananchi wanaoipinga CCM.