![](http://eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/field/image/ccm arusha.jpg?itok=TPybxW8J×tamp=1472533179)
Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha kimetishia kuwafukuza na kuwafuta uanachama viongozi wake wanaoanza kutengeneza makundi ya uchaguzi badala ya kushughulikia matatizo ya wananchi, tatizo ambalo limeshaanza kuleta dalili za kukigawa chama hicho.
Akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali katibu wa chama hicho mkoa wa Arusha bw, Alfonce kinamhala amesema wapo viongozi na wanachama ambao badala ya kujishughulisha na matatizo ya wananchi na kutekeleza ilani ,wanatumia muda wao kupanga makundi na kujiandaa kugombea nafasi jambo ambalo chama hakiwezi kulifumbia macho.
Baadhi ya viongozi wa wilaya akiwemo mwenyekiti wa CCM wilaya ya Monduli Reuben Olle Kuney wamesema tatizo hilo lipo na ni kubwa zaidi katika ngazi ya kata na kwamba limejitokeza wazi wazi wakati wa chaguzi za serikali za mitaa.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa kata wanaotuhumiwa wamewalaumu viongozi wa ngazi za juu za chama hicho kuwa ndio wanaosababisha matatizo yaliyopo sasa likiwemo la kuondoa majina ya wagombea wanaopendekezwa na wana nchi na kuweka watu wao .
Baadhi ya wananchi wakiwemo wa wilaya ya Monduli wamesema pamoja na chama hicho kutekeleza ahadi zake kwa kiasi kikubwa, kasi ya utendaji wa viongozi wake imekuwa ikipungua siku hadi siku kadri muda wa uchaguzi unavyokaribia