Monday , 2nd Feb , 2015

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Francis Cheka, amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu, sambamba na kutakiwa kulipa shilingi milioni moja kama gharama za matibabu na fidia, baada ya kupatikana na hatia ya shambulio la kudhuru mwili.

Francis Cheka Akipanda gari ya Polisi kuelekea Gerezani

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Francis Cheka, amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu, sambamba na kutakiwa kulipa shilingi milioni moja kama gharama za matibabu na fidia, baada ya kupatikana na hatia ya shambulio la kudhuru mwili dhidi ya meneja wa baa yake ya Vijana Social, Bahati Kabanda, mkazi wa Morogoro.

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu mkazi mwandamizi katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro, Said Msuya, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mashitaka, ambapo bila shaka umemtia hatiani mshtakiwa kama alivyokuwa akishtakiwa ambapo hakimu Msuya amedai kutoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na wegine wanaojichukulia sheria mikononi.

Awali imedaiwa na mwendesha mashtaka atuganile Msyani kuwa, mshtakiwa ametenda kosa hilo mnamo Julai 02 mwaka jana, maeneo ya Sabasaba manispaa ya Morogoro, ambapo bila halali na akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria, alimpiga kwa ngumi maeneo ya kichwani na tumboni,Bahati Kabanda maarufu kama Masika, aliyekuwa meneja wa baa yake ya Vijana Social, na kumsababishia maumivu makali, tukio linalodaiwa kufanywa  baada ya  Cheka kudaiwa kutoridhishwa na mahesabu ya mauzo.

Hata hivyo alipopewa fursa ya kujitetea na mahakama, Cheka alishindwa kufanya hivyo na badala yake kuieleza mahakama kufanya kile itakachokuwa imeamua,na hakimu kumpa adhabu hiyo ya miaka mitatu jela na akimaliza kifungo alipe fidia ya shilingi milioni moja kama fidia na malipo ya gharama za matibabu kwa mlalamikaji, kabanda.