Wednesday , 9th Mar , 2016

Mke wa Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), 2015 Mama Regina Lowasa, ameongoza wanawake wa Bawacha kufanya usafi katika hospitali ya wazazi ya Mafiga Manispaa ya Morogoro.

Mama Regina Lowassa, mke wa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa

Wakizungumza na wanawake katika viwanja vya Hospitali hiyo mara baada ya zoezi la usafi mama Regina Lowasa, amewaomba wanawake kote nchini kutokata tamaa juu ya ugumu wa maisha huku mbunge wa viti maalumu mkoa wa Morogoro mhe. Devota Minja akieleza lengo la kutoa vifaa tiba katika hospitali hiyo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema,(BAWACHA), taifa Mhe. Halima Mdee amesisitiza vifaa tiba vilivyotolea vitumike bure kwa wanawake huku Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga akiwakumbusha wanawake kuwapeleka shule watoto wakike ili wapate elimu na kufikia dhana ya hamsini kwa hamsini.

Hata hivyo mganga mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Sufian Msuya amesema hospitali hiyo inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa chumba cha upasuaji hali inayohatarisha maisha ya wanawake wanapohitaji huduma hiyowakati wa kujifungua.

Zoezi hilo la kufanya usafi katika hospitali ya wazazi ya Mafiga limeshirikisha wanawake wa Bawacha wa mji wa Morogoro, viongozi wakuu wa kitaifa wa Baraza hilo, wabunge wa viti maalumu wa Chadema Mikoa ya Morogoro na Dodoma pamoja na viongozi wa Manispaa ya Morogoro wakiongozwa na Mstahiki Meya Pascal Kihanga.