Wednesday , 24th Feb , 2016

Baraza la Watoto laitaka serikali iangalie upya mfumo wa elimu na mitaala inayotumika kufundishia iwapo inaendana na wakati ulioko na kuwawezesha watanzania kukabiliana na changamoto za kijamii,kiuchumi na kisiasa zilizopo .

Mwenyekiti wa Baraza la Watoto wilaya ya Arusha, Hassan Omari Kimaro

Mwenyekiti wa Baraza la Watoto wilaya ya Arusha, Hassan Omari Kimaro, amesema kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na serikali katika masuala ya elimu bado kuna changamoto nyingi zinazoikabili elimu ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi.

Mbali na hitaji la kuangalia upya mfumo wa elimu wameiomba serikali ianzishe vyama vya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili waweze kupaza sauti zao na kutetea haki zao hasa ukizingatia kuwa wao ndio waathirika wakubwa mitaala na mabadiliko yanayotokea kwenye mfumo wa elimu

Mjumbe wa Baraza hilo Brina Salvatory amesema kuwa kiwango cha ufaulu katika shule za sekondari kimepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na shule binafsi hivyo serikali na wadau wa elimu wana jukumu la kujenga mazingira bora yatakayoinua kiwango cha elimu.

Katibu wa Baraza la Watoto Raphael Denis amesema kuwa wamepanga kuanzisha mbio za mwenge za kutetea haki za watoto zitakazohitimishwa katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Watoto nchini wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo watoto wa mitaani,ukosefu wa viwanja vya kutosha vya michezo .