Monday , 9th Feb , 2015

Bandari bubu zipatazo 45 zilizobainika kuwepo katika vijiji mbalimbali vilivyopo katika fukwe za bahari ya hindi katika wilaya nne za mkoa wa Tanga, zimebainika kusafirisha bidhaa mbalimbali za magendo.

Bandari bubu zipatazo 45 zilizobainika kuwepo katika vijiji mbalimbali vilivyopo katika fukwe za bahari ya hindi katika wilaya nne za mkoa wa Tanga, zimebainika kusafirisha bidhaa mbalimbali za magendo pamoja na dawa za kulevya kwenda nje ya nchini na kisiwani pemba kwa kutumia ngalawa na boti, hatua ambayo inaikosesha serikali kiasi kikubwa cha mapato.

Uchunguzi uliofanywa na EATV na kuthibitishwa na wadau wa mamlaka za usafiri mkoa wa Tanga katika bandari bubu ya Kigombe iliyopo katika fukwe za bahari ya Hindi wilayani Muheza, afisa mfawidhi wa mamlaka ya usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) Walukani Luhamba pamoja na wasafirishaji wa vyombo vya majini wamesema bidhaa zao husafirishwa pamoja na abiria kwenda Unguja na Pemba hasa nyakati za usiku.

Awali wakiwa katika operesheni ya kukagua baadhi ya vyombo ambavyo husafirisha bidhaa na abiria bila kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na serikali, afisa mfawidhi kituo cha usimamizi wa rasilimali kanda ya kaskazini Tanga Obadia Ngogo, uchunguzi uliofanywa katika bandari bubu umeonesha kuwa baadhi ya wamiliki wenye vyombo vya usafiri wameweka namba bandia za usajili katika vyombo vyao ili waweze kukwepa kodi kwa serikali.

Kufuatia hatua hiyo serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi imeingia mkataba na wadau wa kampuni za uvuvi kutoka Afrika ya kusini kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya nne nchini kwa ajili ya kuweka nembo maalum katika vyombo vyao ili kuzuia ulaghai unaofanywa na baadhi ya wasafirishaji wa kukwepa kulipa shilingi 17,000/= kila mwezi kwa serikali.