Thursday , 24th Nov , 2016

Asilimia 50 ya wananchi waliohojiwa katika utafiti wa kubainisha ubora wa elimu katika shule za serikali tangu kuanzishwa kwa mpango wa elimu bila malipo, wamekiri elimu hiyo kuwa na ubora.

Mkurugenzi Mkuu wa Twaweza, Aidan Eyakuze

Mkurugenzi mtendaji wa TWAWEZA Aidan Eyakuze amesema idadi hiyo ni ya wananchi kati ya 1,806 waliohojiwa Tanzania bara ambapo amesema asilimia 35 wamesema ubora wa elimu umebaki palepale na wengine asilimia 15 wamesema ubora umeshuka kabisa.

Vilevile asilimia 60 ya wananchi wameonesha kutamani kuwasomesha watoto wao katika shule binafsi.

Utafiti huo pia umebainisha kuwa asilimia 34 ya wananchi wamelalamikia ukosefu wa waalimu, asilimia 30 wamelalamikia ukosefu wa madawati na asilimia 13 wakilalamikia ukosefu wa  madarasa, wengine wakilalamikia ufundishaji na ukosefu wa chakula kwa wanafunzi.

Adha tafiti hiyo pia imebaini kuwa asilimia 85 ya wazazi hawajihusishi na masuala ya masomo ya watoto wao, huku asilimia 83 imekuwa ni changamoto za miundombinu na matokeo mabaya ya wanafunzi na utovu wa nidhamu kwa wanafunzi

Utafiti huo umefanyika kati ya Agosti 7 na 14 mwaka huu hata hivyo baadhi ya wasomi walioshiriki uwasilishwaji wa ripoti hiyo kutoka chuo kikuu cha elimu wamesema matokeo hayo hayaendani na uhalisia wa hali ya elimu nchini na kwamba elimu haiwezi kuwa na ubora kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee.