Thursday , 9th Jun , 2016

Mtuhumiwa Isack Habakuki amehukumiwa jana na Mahakama ya hakimu Mkazi Arusha, kulipa faini ya Sh. Milioni 7, baada ya kupatikana na kosa la kumwita Rais Dk.Magufuli kuwa ni bwege kupitia mtandao wa kijamii.

Mtuhumiwa Isack Habakuki aliemtusi rais Magufuli akiwa chini ya Ulinzi wa Polisi.

Akisoma hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Augustine Rwizile, alisema kuwa mshitakiwa huyo kwa kuwa ni kosa la mara ya kwanza na pamoja ametetewa na wakili wake Moses Mahuna kuwa anafamilia inayomtegema na amekiri kosa, hivyo hajasumbua mahakama kwa maana hiyo apungiziwe adhabu, lakini mahakama inamtia hatiani.

Hakimu Rwiziele amesema kwa kuwa mshitakiwa amekiri kuandika maneno hayo ambayo siyo maadili na kupotoshoa umma na hata mtoto wake hawezi kumwita bwege, hivyo ili iwe fundisho kwa wengine kutumia vizuri mitandao ya kijamii inamuhumu kulipa faini hiyo kwa awamu mbili Julai 8 na Agosti 8 mwaka huu awe amemaliza, endapo atashindwa ataenda Jela miaka mitatu.

Amesema sheria zilizopo zinatengenezwa ili kulinda jamii na kosa alilofanya linaudhi jamii, hivyo bora alipe faini hiyo ili ajifunze kutumia vema mitandao ya kijamii.

Aidha simu yake aina ya tekno aliyotumia kutuma ujumbe huo wa kuudhi kwenye mitandao ya kijamii, imetaifishwa kwa sababu ndio iliotumika kuudhi watu.

Kabla ya hukumu hiyo kutolewa Wakili wa serikali, Vitalisi Timoni, aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa huyo aliandaika ujumbe huo Machi 17 mwaka huu na walipofanya utafiti walimbaini yeye na alikamatwa na kuhojiwa kituo cha Polisi Osterbei Dar es Salaam na alikiri kuandika ujumbe huo.

Amesema mshtakiwa aliandika katika mtandao wake wa kijamii Face Book kuwa hizi ni siasa za maigizo alafu mnamlinganisha na Nyerere wapi bwana, lugha iliyoudhi watu wa mitandao ya kijakii wengi na ndipo Mamlaka ya mawasiliano TCRA ilipomtafuta kwa ushirikiano na Polisi na kumkamata.

Hata hivyo wakili wake aliyekuwa akimtetea Moses Mahuna, aliomba mahakama kumpunguzia adhabu sababu ni kosa la mara ya kwanza na anategemewa na familia, lakini pia haijasumbua mahakama kwa kukiri kosa, hivyo bora apewa ahabu ndogo kama kulipa faini ili aendelee kujenga taifa.

Mshitakiwa baada ya kuhumiwa alikubali kulipa faini hiyo ya shilingi milioni saba kwa miezi miwili na yupo nje.