Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Tonia Kandiero aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo,
Kandiero amepandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Ukanda wa Kusini mwa Afrika katika ofisi zake zilizopo Afrika Kusini.
Rais Magufuli amemshukuru Dkt. Tonia Kandiero kwa juhudi kubwa alizozifanya akiwa Mwakilishi Mkazi wa AfDB hapa nchini ambapo miradi mikubwa na muhimu katika maendeleo imetekelezwa na inaendelea kutekelezwa.
Akizungumza baada ya kuagana na Rais Magufuli Dkt. Tonia Kandiero amemshukuru Rais Magufuli na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano alioupata katika kipindi cha miaka 6 aliyokuwa hapa nchini na amesema anaondoka akiwa ameiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa ya kimahusiano na AfDB ambapo miradi yenye thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 2 (zaidi ya shilingi trilion 4 za kitanzania) imetekelezwa hususani katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo anayemaliza muda wake baada ya kuiwakilisha nchi ya Cuba kwa miaka minne.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi wa Cuba anayemaliza muda wake hapa nchini George Luis Lopez Tormo aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga
Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo kwa uhusiano na ushirikiano mzuri aliouendeleza kati ya Tanzania na Cuba uliojengwa na waasisi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mhe. Fidel Castro wa Cuba
Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo amemshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Cuba na amesema anaondoka akiwa anaamini kuwa uhusiano kati ya nchi hizi utaendelea kuwanufaisha wananchi ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo na huduma za kijamii.






