Nusu ya wananchi wa Tanzania Bara sawa na 53% wamesema hawafahamu kilichojiri Zanzibar tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.
Kwa muibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza yameonesha kuwa, wananchi 4 kati ya 10 sawa na 43% wana taarifa kuwa uchaguzi mpya ulifanyika Machi 20 2016 ambapo 39% wanafahamu kuwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba yalifutwa.
Kadhalika wananchi wa Tanzania Bara wametoa maoni yao kuhusu nini kifanyike kutatua mgogoro uliopo, ambapo takriban nusu ya wananchi, 42%, wamesema Rais aliyechaguliwa kwenye uchaguzi mpya wa Machi 20 2016 atambulike kuwa Rais halali, huku 20% pekee wamesema uchaguzi mpya wa tarehe 20 Machi ulikuwa ni hatua nzuri ya kutatua mgogoro.
Baadhi ya mapendekezo ya wananchi kwenye utafiti huo ni 14% wamependekeza mgombea urais wa Chama cha CUF, Seif Shariff Hamad, kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 2015, 13% wanataka iundwe serikali ya umoja wa kitaifa na 8% wamependekeza yafanyike mazungumzo kutafuta ufumbuzi wa amani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza , Aidan Eyakuze amesema, Serikali ya Muungano, na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina kazi kubwa ya kurejesha umoja baina ya wapiga kura visiwani Zanzibar, lakini pia, inatia wasiwasi kubaini kwamba idadi kubwa ya watanzania walikiri kutojua kilichotokea Zanzibar baada ya uchaguzi wa Oktoba 2015.

