Monday , 14th Sep , 2015

Polisi Mkoa wa Dodoma Inawashikilia watu wanne na inaendelea kuwatafuta wengine kutokana na tuhuma za kujeruhi, kuharibu mali na Kufanya fujo kwenye msafara wa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM Anthony Mavunde.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, David Misime tukio hilo Septemba 11 majira ya saa 18:30 ambapo wanachama na wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wanatoka kwenye mkutano wa kampeni uliokuwa umehutubiwa na viongozi wa CHADEMA akiwepo Mh. Edward Lowassa katika viwanja vya Barafu walipofika maeneo ya njia panda ya NAM Hotel Dodoma walianza kuwatukana na kuwashambulia kwa mawe wanachama na wafuasi wa CCM waliokuwa wanatokea kwenye mkutano wa kampeni maeneo ya Msalato.

Kutokana na vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na sheria, kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi walisababisha watu wanne kupata majeraha na magari manne kupata uharibifu wa kuvunjwa vioo.

Misime amesema kuwa watuhumiwa wengine wanaendelea kutafutwa ili wote waweze kufikishwa mahakamani.

Aidha ametoa wito kwa viongozi wa vyama wawaelimishe wanachama na wafuasi wao kujiepusha na vitendo kama hivi ambavyo ni kinyume na sheria, kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi.

Pia watambue wanapokwenda na kurudi kwenye mikutano ya kampeni barabara wanazotumia bila kufuata sheria wanawatia hofu na kuwanyima haki watu wengine wanaotumia barabara hizo.

Pia wawaelimshe wanapokutana na wenzao wa vyama vingine waache kutumia lugha chafu, kuwafanyia vurugu, kupiga na kuharibu mali.

Amesema hali hii ni kutokana na baadhi yao kutumia waendesha bodaboda ambao huendesha pikipiki zao kwa fujo na kuyumba barabara nzima jambo linalowafanya watumiaji wengine kushindwa kutumia huduma hii bila karaha.

Amesema Jeshi la Polisi Dodoma litaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaoacha kutii sheria, kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi.