Sunday , 27th Jan , 2019

Mbunge Ahmad Katani (CUF) wa jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara, ameweka wazi juu ya kile kinachoendelea kuhusu malipo ya pesa za korosho kwa wakulima wa zao hilo.

Akizungumza na www.eatv.tv, Katani amesema kwamba licha ya kauli ya Rais kutaka watu walipwe pesa zao kwakuwa pesa ipo, lakini ukweli ni kwamba wakulima wengi hawajalipwa na watu wanaogopa kuzungumza ukweli juu ya kile kinachoendelea kwa kuogopa kufukuzwa kazi.

Katani ameendelea kufafanua kwamba watu waliolipwa pesa hizo ni wachache mno huku akitolea mfano jimboni mwake Tandanimba ambako ndio kunaongoza kwa uzalishaji wa Korosho kwa mikoa ya kusini, ameweka wazi kuwa waliolipwa hawazidi asilimia 40 huku akiwataka watu wawe wakweli kwa kuacha maigizo ya juu ya malipo ya pesa zao hilo.

“Watu wanaficha ukweli sababu ya uoga, watu wengi wanataka kutetea uongo uwe ukweli kwa uoga,  kwa mfano mimi jimboni kwangu waliolipwa si zaidi ya asilimia 40, na wengi waliolipwa ni wale wasiozidi tani 1.5, wenye kilo kuanzia 1,600 wengi wao hawajalipwa”, amesema Mbunge Katani.

Katani ameendelea kuelezea, "kama pesa ipo kwa nini watu hawalipwi?. Ziko wapi?, jamaa anatengeneza sinema ya mtu mmoja, na watu wengi wanaogopa kuwa 'fired' wakisema ukweli, watu hawajalipwa, acheni sinema za kwneye mitandao, watu wanakuwa waongo”.

Hivi karibuni Rais Magufuli alitoa tena maagizo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akitaka wakulima walipwe pesa za korosho, jambo ambalo limekuwa likiibua sintofahamu kwenye jamii ya wakulima wa zao hilo.