Jumatano , 29th Aug , 2018

Meneja wa msanii wa bongo fleva, Snura Mushi maarufu kama Malkia wa uswazi, HK amefunguka na kudai hana taarifa zozote na mwanadada huyo kuwa na ujauzito, huku akisisitiza kwamba endapo itakuwa ni kweli basi atafurahi kupata mjukuu mwingine wa tatu.

Snura

HK amebainisha hayo alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha eNewz inayorushwa na tinga namba moja kwa vijana EATV, baada ya kuenea uvumi kuwa Snura ana ujauzito mwingine ambapo inasemekana ni wa mpenzi wake ambaye pia ni msanii wa bongo fleva Minu Calipto. 

"Kwa jinsi ninavyomjua Snura ni mtu ambaye hajawahi kutoa ujauzito wala hajawahi kufikiria kufanya hivyo, kwa hiyo kama ni kweli kapata ujauzito basi nategemea kupata mjukuu wa tatu", amesema HK.

Mbali na hilo, HK amedai haitokuwa rahisi kwa Snura kushuka kimuziki ikiwa kweli amekusudia kupata ujauzito.

Meneja wa Snura, HK

"Sidhani kama ataweza kushuka kimuziki kwasababu yule ni mwanamke halafu ni nguzo katika kuisaidia familia yake. Hivyo haitakuwa rahisi kwa yeye kujibweteka, Snura katoka kuzaa juzi tu mtoto wa pili na hata akitaka kuzaa wanne haina tatizo", amesisitiza HK.

Kwa upande mwingine, anayedaiwa kuwa na mahusiano na Snura mnamo Agosti 16 mwaka huu aliuthibitishia umma kuwa ni kweli mpenzi wake anaujauzito na muda wowote anaweza kujifungua na kuitwa baba.