
Hans van der Pluijm
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF Alfredy Lucas amesema Kocha wa Yanga Hans van der Pluijm amefungiwa mechi tatu na faini ya shilingi laki tano mara baada ya kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa katika mchezo namba 59 dhidi ya Ruvu Shooting.
Alfred amesema klabu ya Yanga pia imepigwa faini ya shilingi laki tano baada ya mashabiki wake kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa walipokuwa wakiingia vyumbani wakati wa mapumziko.
“Timu ya Ruvu Shooting imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 12, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu”, amesema Alfredy Lucas.
Alfred amesema Kocha wa Azam FC, Zeben Hernandez naye amefungiwa mechi tatu na faini ya shilingi laki tano mara baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (ordered off) kwa kukataa kuheshimu mipaka ya eneo la ufundi (technical area) katika mechi dhidi ya Mbao FC.
Kocha wa Azam FC - Zeben Hernandez
Alfred amesema klabu ya Simba nayo imepigwa faini ya shilingi laki tano kutokana na timu yake kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons na kufika wakati taratibu zote za msingi zikiwa zimemalizika.
“Klabu zote (Tanzania Prisons na Simba) zimepigwa faini ya shilingi laki tano kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa milango isiyo rasmi”, amesema Alfred .
Alfredy amesema ameongeza kuwa Tanzania Prisons imepigwa faini ya shilingi laki tano baada ya gari la Jeshi la Magereza namba MT 0084 aina ya Toyota Land Cruiser Pick Up likiwa na watu 15 kuingia uwanjani kwa nguvu, na kusababisha kupigwa na kuumizwa kwa mlinzi wa getini.
“Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kutoka Morogoro amepewa onyo kali kwa kutoripoti baadhi ya matukio ya wazi yaliyotokea kabla ya mechi hiyo kuanza”, amesema Alfredy.
Wachezaji wa Prisons wakishangilia bao katika mechi yao dhidi ya Simba
Alfred amesema katika mechi ya Ndanda FC dhidi ya Stand United kadri muda ulivyokuwa ukienda waokota mipira (ball boys) walichelewesha kurudisha mipira uwanjani, na mbaya zaidi mipira ilikuwa ikifichwa kiasi cha kubaki miwili kati ya sita iliyokuwepo. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ili ahakikishe suala hilo halijitokezi tena.
Alfred amesema katika mchezo wa Ruvu Shooting dhidi ya Ndanda FC, timu ya Ndanda imepigwa faini ya shilingi laki tano kwa kosa la timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi.
Alfred ameongeza kuwa, Ruvu Shooting pia ambayo ilikuwa uwanja wa nyumbani, imepigwa faini ya shilingi laki tano kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 15.
Alfred Lucas
Alfred amesema, katika mchezo uliozikutanisha Mwadui FC dhidi ya Simba SC, klabu zote mbili zimepigwa faini ya shilingi laki tano kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango wa mashabiki, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni.
Alfred ameongeza kuwa klabu ya Toto Africans imepewa onyo kali kutokana na timu yake kuchelewa kufika uwanja kwa dakika saba katika mchezo wao dhidi ya Simba SC
Said Kipao - Kipa wa JKT Ruvu
Alfred amesema, wachezaji wa JKT Ruvu, ambapo ni Mlinda Mlango Said Kipao, Samwel Kamuntu (22), Pela Mavuo (16) na Paul Mhidzhe (23) wamefungiwa mechi tatu na faini ya shilingi laki tano kila mmoja kwa kuwatukana waamuzi baada ya mchezo dhidi ya Majimaji kumalizika.