Jumatano , 29th Aug , 2018

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania,Taifa Stars ,Emmanuel Amunike amewatimua wachezaji sita kutoka katika klabu ya Simba ambao wameshindwa kuwasili katika kambi ya timu ya Taifa inayojiwinda na mechi ya kundi L dhidi ya Uganda ambayo ni ya kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika AFCON.

Akitangaza mabadiliko hayo katika mkutano na wanahabari kwenye ofisi za shirikisho la soka hapa nchini TFF zilizopo Karume jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfried Kidau amesema.

Kambi imeanza rasmi jana lakini kwa masikitiko wachezaji walioko kambini ni wachezaji wa klabu ya Azam na mchezaji mmoja wa Simba, Aishi Manula “.

Baada ya jana kuambiwa taarifa hizo niliwasiliana na viongozi wa Simba, Meneja wa timu na baadaye nikaongea na baadhi ya wachezaji nikiwasisitiza umuhimu wa timu ya taifa na kocha aliongeza muda hadi saa 12 asubuhi ya leo kwa wachezaji hao kuwasili kambini lakini hadi muda huo hawakuwasili “. Ameongeza Kidau.

Wachezaji wa Simba walioachwa ni pamoja na Erasto Nyoni, Hassan Dilunga, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, John Bocco na Shiza Kichuya.

Aidha Kidau amesema kuwa maamuzi hayo ya kuwaondoa wachezaji wa Simba ni msimamo wa kocha na wao kama viongozi wa juu wa shirikisho wameunga mkono uamuzi huo katika kuhakikisha nidhamu inazingatiwa na kusisitiza kuwa hakuna klabu wala mchezaji yoyote aliye juu ya timu ya taifa.

Wachezaji walioitwa timu ya taifa kuchukua nafasi hizo 6 za wachezaji wa Simba SC waliondolewa baada ya kuchelewa kuripoti kambini ni, Paul Ngalema, Salumu Kimenya, David Mwantika, Salumu Kihimbwa, Ali Abdulkadir, Kelvin Sabato na Frank Domayo.

Kambi ya Taifa Stars imeanza jana huku wachezaji wanaocheza soka la kimataifa wakitarajia kujiunga na kambi hiyo kuanzia Septemba 4 kutokana na kuwa katika majukumu ya klabu zao katika kipindi hiki. Mchezo huo unatarajiwa kutachezwa 8, Septemba jijini Kampala Uganda.