Jumanne , 12th Jun , 2018

Kuelekea Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, kocha wa Ufaransa Didier Deschamps huenda akaingia kweney rekodi ya kuwa kocha wa tatu aliyechukua ubingwa wa dunia akiwa mchezaji na baadae kama kocha.

Deschamps ambaye anainoa Ufaransa, alikuwa mchezaji na nahodha wa timu hiyo wakati inachukua ubingwa wa Dunia kwa kuifunga Brazil 3-0 mwaka 1998 kwenye fainali zilizofanyika nchini kwao. 

Makocha ambao wamewahi kuweka rekodi ya kuchukua ubingwa wakiwa na timu zao kama wachezaji na baadae kutwaa wakiwa makocha ni Mario Zagallo alichukua kama mchezaji mwaka 1958 akiwa na Brazil kabla ya kuchukua akiwa kocha wa Brazil mwaka 1962.

Kocha mwingine ni Franz Beckenbauer wa Ujerumani ambaye alitwaa ubingwa akiwa mchezaji wa timu hiyo mwaka 1974 na kisha mwaka 1990 kama kocha wa taifa hilo. 

Katika timu 32 zinazoshiriki fainali hizo mwaka huu hakuna kocha ambaye ameshachukua ubingwa wa dunia akiwa mchezaji zaidi ya Didier Deschamps wa Ufaransa. Endapo Deschamps atachukua ubingwa ataingia kwenye kundi la Mario Zagallo na Franz Beckenbauer.