Jumatano , 8th Jun , 2016

Siku moja baada ya mlinzi wa kati wa Mtibwa Sugar, Andrew Vicent 'Dante' kusaini mkataba wa miaka miwili Jangwani, Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amesema kuwa siyo huyo tu wakitaka wabomoe kikosi kizima na Mtibwa itabaki palepale.

Maxime aliongeza kuwa kuondoka kwa 'Dante' si ajabu wala pengo kikosini kwake kwani ana fursa za kutosha kupata mbadala wake, ikiwemo michuano ya Ndondo Cup inayoendelea katika viwanja mbalimbali jijini Dar kwani naye alichukulia hukohuko alipokuwa daraja la pili kwenye timu ya Kariakoo Lindi ya Mtwara.

"Mwenyewe nilimuokota daraja la pili, nikamtengeneza msimu mmoja tu, akaitwa timu ya taifa (chini ya kocha Mart Nooij), leo anasajiliwa Yanga, sina shaka naamini kina Dante ni wengi sana Tanzania hii, hata kwenye Ndondo Cup naweza kuwapata wengi tu."

"Wao wabomoe tu, wakitaka wachukue wote, Dante siyo pengo kwetu na mbadala wake atapatikana tu mwishoni mwa usajili, kama yeye miaka miwili tu amefanikiwa kwenye timu kubwa, nini kinashindikana kupata mbadala wake?" alisema maxime

Nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars amesema hayo kutokana na timu kubwa za Yanga, Simba kuigeuza Mtibwa kama akademi yao.