
Ras Ino ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kueleza kwamba ili msanii huyo asishuke ni lazima abadilike kulingana na soko la muziki na kuwekeza zaidi.
"Kuchepuka ili kulifuata soko linataka ili kujikubalisha ni kitu muhimu sana, tofauti na wengi wanavyofikiria kwa mfano mambo tanzu ya pembeni yasiyohusiana na muziki kwa mfano hizi skendo wanazoziunda ambazo hazina kichwa wala miguu, utaona kama zinakuweka kwenye masikio ya watu lakini kwa namna moja au nyingine, utakapoishiwa mbinu vya pembeni vya kimuziki na muziki ukadorola lazima utashuka", alisema Ras Ino.
Pamoja na hayo Ras Inno amesema wasanii wengi wanabweteka baada ya kupata mafanikio na kusahau changamoto ambazo zitamkabili.
"Mara nyingi inatokea kitu kimoja kwanza kwenye kukubalika, watu kunakuwa na kule kujisahau kwa sababu ustaa haukugongei hodi au mafanikio hayakugongei hodi, unakuta tu ghafla juhudi za muda mrefu ulizozifanya unafika kwenye kiwango unakubalika, lakini kama mwenyewe hujitambui, unakuta unabweteka, lakini anachokosea anasahau kuwa kuna changamoto, kwamba kuna watu wanakuja na nini kitambakisha shabiki aendelee kukusikiliza wewe", alisema Ras Inno.