Jumanne , 27th Sep , 2022

Klabu ya Yanga imemtangaza Mzambia Andre Mtine kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili akichukua mikoba ya Senzo Mbatha Mazingisa aliyeondoka klabuni hapo miezi iliyopita baada ya mkataba wake kumalizika.

Andre Mtine Mtendaji mkuu mpya wa Klabu ya Young Africans SC

Utambulisho wa Mtendaji huyo mpya, umefanywa na Rais wa klabu ya Yanga Injinia Hersi Said ambaye amesema wanaamini kuwa uzoefu wa Mtine utaongeza thamani ndani ya klabu na kuleta mafanikio ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

''Huu ni muendelezo wa ajenda yangu kubwa katika uongozi wangu ambayo ni kuimarisha kila idara kwa kuleta watu wenyewe weledi wa kufanya kazi za Yanga'' amesema Hersi

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu huyo mpya wa Yanga Andre Mtine amesema amejiunga na Yanga kwa kuwa ni klabu kubwa na yenye historia barani Afrika huku akitoa rai kwa wanachama na mashabiki wa Yanga kushirikiana ili kusaidia kufikia malengo makubwa ya klabu.

"Yanga ni timu kubwa sana, nimekuwa naifuatilia kwa muda sasa. Nimejifunza kuwa ni timu kubwa, na tunaweza kuifanya kuwa kubwa zaidi, siyo tu ukanda wa Afrika Mashariki bali kuwa klabu kubwa zaidi Afrika," amesema Mtine

Mzambia Andre Mtine alianza kujihusisha na michezo tangu mwaka 1988 na kupita klabu kama Zesco, Power Dynamo, Bidco pamoja na TP Mazembe aliyodumu nayo kwa miaka 12 sambamba na kushika nafasi ya ujumbe wa kamati ya Fedha ndani ya CAF.