Jumatatu , 23rd Nov , 2020

Mshambuliaji wa klabu ya AC Milan na gwiji wa timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic amefunga mabao mawili dhidi ya SSC Napoli kwenye mchezo wa Serie A usiku wa hapo jana nakuisaidia klabu yake kupata ushindi wa mabao 3-1 na kutamba kileleni mwa msimamo wa Serie A.

Zlatan Ibrahimovic (Katikati) akipongezwa na mlinzi Theo Hernandez (Kulia) baada ya kupachika bao katika mchezo dhidi ya Napoli.

Zlatan amepachika bao la kwanza dakika ya 20 bao lililopikwa na mlinzi wa kushoto Theo Hernandez kabla ya kuweka wavuni bao la pili dakika 34 baadaye na kuwapa uongozi mnono na dakika ya 63 mshambuliaji wa Napoli Dries Mertens aliifungia timu yake bao la kufutia machozi.

AC Milan wakatumia vizuri mwanya wa SSC Napoli kuwa na wachezaji pungufu kufuatia kiungo Tiemuoe Bakayoko kuoneshwa kadi nyekundu baada ya kucheza sivyo ndivyo na kuongeza bao la tatu dakika za nyongeza lililowekwa kimiani na Jens Petter Hauge.

Baada ya dakika tisini kumalizika, AC Milan wameondoka na ushindi mkubwa ugenini na kuwafanya wawe vinara kwenye msimamo wa Serie A kwa kufikisha alama 20 katika michezo 8 waliyocheza wakishinda michezo 6 bila kupoteza mchezo hata mmoja wakiwa na sare mbili.

Mabao ya Zlatan yanafanya mshambuliaji huyo kuongoza jahazi la wachezaji wanaoongoza kuwa na mabao mengi msimu huu akiwa na mabao 10 na kutengeneza bao 1 kwenye michezo 6 aliyocheza akifuatiwa na CR7 mabao 8 na Romelu Lukaku akishika watatu akiwa na mabao 7.

Kiwango cha Zlatan kinaendelea kuwa gumzo kwa wafuatiliaji wa soka ulimwenguni na kudai 'Hakamatiki' wakistaajabu ubora anaouonesha mshambuliaji huyo klabu yeyote aendapo lakini kubwa zaidi ni kuwa na umri mkubwa wa miaka 39 na kuisaidia AC Milan kuanza ligi vyema.

Ikumbukwe kuwa msimu wa mwaka 2012 AC Milan walikuwa mabingwa wa Serie A msimu ambapo Zlatan Ibrahimovic alikuwa anaichezea klabu hiyo na baadaye kutimkia klabu ya PSG ya Ufaransa, Manchester United ya Uingereza, LA Galaxy ya Marekani na kurejea AC Milan msimu uliopita.