Alhamisi , 15th Oct , 2020

Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Yusuph Mhilu aliendeleza kasi ya kucheka na nyavu msimu huu ambapo jana alifunga bao lake la tatu katika mechi tatu alizocheza licha ya timu yake kupoteza mbele ya Namungo kwa bao 2-1 katika mchezo wa raundi ya tatu ligi kuu ya Tanzania bara.

Mshambuliaji machachari wa Kagera Sugar, Yusuph Mhilu ambaye amekua katika kiwango bora kwa msimu wa pili mfululizo katika VPL.

Mhilu ambaye alijiunga na Kagera Sugar msimu juzi, akitokea Ndanda alipokua akicheza kwa mkopo, ameanza vyema kampeni ya kupachika mabao mfululizo ingawa bado hajapewa nafasi ya kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania.

Msimu uliopita nyota huyo alifunga mabao 16 na pasi 4 za usaidizi wa mabao ambapo alisaidia Kagera Sugar, kumaliza katika nafasi ya 8 kwenye msimamo wa VPL.

Nyota huyo ni miongoni mwa wachezaji wazawa wenye mabao mengi katika ligi kuu, lakini bado hazungumzwi sana juu ya kiwango chake kiasi cha wadadisi wa mambo kuhisi kwamba ili apate nafasi katika timu ya taifa labda ni lazima ucheze katika vilabu vya Simba, Yanga au Azam.

Akizungumzia juu ya kiwango cha nyota huyo, mchambuzi wa michezo kutoka East Africa Radio, Ayoub Mgando amesema ni vigumu sana kwa wachezaji aina ya Yusuph Mhilu kujumuishwa katika kikosi cha Taifa Stars kwasababu wengi hutazama wachezaji wanaozitikisa Simba au Yanga jambo ambalo pengine ni mtazamo hasi kwa maendeleo ya mpira wa miguu.

Kinda huyo aliyekulia mitaa ya Twiga na Jangwani, amefunga mabao mengi kuliko hata washambuliaji wa Yanga waliosajiliwa kwa fedha nyingi wakiwemo Michael Sarpong kutoka Ghana, Yacouba Sogne kutoka Burkinafaso ambao hadi sasa wamefunga bao moja kila mmoja.