Yanga yatangaza Kaimu Katibu Mkuu mpya

Ijumaa , 20th Nov , 2020

UongozI wa Klabu ya Yanga, leo Novemba 20 umemtangaza Haji Mfikirwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya wakili Simon Patrick ambaye amesimamishwa kutokana na tuhuma za kuihujumu timu.

Haji Mfikirwa Kaimu Katibu Mkuu mpya wa Yanga SC

Mfikirwa ametangazwa na Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga Frederick Mwakalebela mbele ya waandishi wa habari. Katika utambulisho huo Mwakalebela amesema Kamati ya Utendaji inamuamini Haji na ataweza kuipeleka mbele klabu hiyo kutokana na uwezo mkubwa alionao.

Haji Mfikirwa anachukua nafasi ya Patrick Simon ambaye alisimamishwa kazi Novemba 18, kutokana na tuhuma za kuihujumu Yanga, ikiwemo kufanya vikao vya siri na viongozi wa mahasimu wao wa soka hapa nchini.

Lakini pia katika mkutano huo na wanahabari Mwakalebela ameliomba Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuzifanyia kazi kesi zao walizo ziwasilisha ikiwemo ile ya Ramadhani Kabwili, pamoja na ile inayohusu juu ya uhalali wa mkataba wa Bernard Morrison na klabu ya Simba.

Aidha Yanga wameomba kesi ya mkataba wa Morrison na klabu ya Simba isikilizwe kabla ya dirisha dogo la usajili halijafunguliwa Disemba 15, 2020 kwani kuna ujanja unaweza kufanyika wa kubadilisha mkataba huo.