Jumanne , 20th Feb , 2024

Uongozi wa Yanga SC umesema utautumia mchezo dhidi ya CR Belouzidad ya Algeria kama njia ya kutimiza malengo yao ya kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye mchezo unaotaraji kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa mnamo Jumamosi ya Februari 24-2024.

Afisa Habari wa Yanga SC Ally Kamwe amewaomba mashabiki na wapenzi wa Yanga kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuipa hamasa timu hiyo ili waweze kufikia lengo la kufuzu kwenda hatua ya robo fainali huku wakijivunia rekodi kubwa na nzuri pindi wakicheza  kwenye dimba la Benjamin Mkapa

''Mchezo huo utakuwa ni 24/2/2024. Mpango wetu ni robo fainali. Na tutautimiza mpango huu kama tutaungana pamoja na kwenda Uwanjani kuwapa nguvu wachezaji wetu siku hiyo''amesema Kamwe

Kwa upande mwingine, Afisa idara ya wanachama na Mashabiki wa Yanga SC Jimmy Shomari Msindo maarufu kama Jimmy Kindoki amesema kuelekea mchezo huo wameupa jina la Pacome Day “Kitaalamu Zaidi” ili kwenda kutimiza azma yao ya kutinga hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika

Yanga SC inataraji kushuka dimbani kesho Jumanne Februari 20,2024 kupambana na Polisi Tanzania kwenye mchezo wa hatua ya 32 bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup(ASFC) kwenye dimba la Chamanzi Jijini Dar es Salaam