Ijumaa , 8th Jan , 2021

Mabingwa mara moja wa kombe la Mapinduzi, klabu ya Yanga inatazamiwa kushuka dimbani kukipiga dhidi ya 'Wauaji wa kusini' klabu ya Namungo ya mkoani Lindi mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Amani saa 2:15 usiku ya leo tarehe 8 januari 2021 visiwani Zanzibar.

Wachezaji wa Yanga na Namungo wakiwa wanamzonga mwamuzi kwenye mchezo wa VPL wa mzunguko wa kwanza msimu huu uliomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye dimba la mkapa jijini Dar es Salaam.

Wachezaji wa Yanga watakaokosekana ni Feisal Salum, Yassin Mustafa, Farid Musa, Ditram Nchimbi na Deus Kaseke waliopo kwenye kambi ya timu ya taifa jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya DR Congo utakaochezwa Januari 12, 2021 saa 11:00 jioni kwenye dimba la mkapa ambayo pia ni matayarisho kuelekeza fainali za CHAN mwaka huu.

Yanga wataingia katika mchezo huo huku kukiwa na taarifa iliyothibitishwa kuwa mlinzi wake wa kati wa kutumainiwa aliye katika kikosi cha Timu ya Taifa, Bakari Mwamnyeto amepata msiba wa mke na mtoto wake hapo jana.

Kwa upande wa Namungo itawakosa Edward Charles Manyama, Carlos Protas na Lucas Kikoti ambao pia wapo kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Taifa Stars.

Licha ya wachezaji hao nyota na tegemezi kwenye vikosi vya timu zote mbili kukosekana lakini mchezo huo unataraji kuendelea kuwa na upinzani mkubwa kutokana na vikosi hivyo kusheheni wachezaji wengi wenye uwezo mzuri wa kushindania alama tatu muhimu.

Mara ya mwisho wawili hawa kukutana ilikuwa ni tarehe 22 Novemba 2020 ambapo mchezo huo wa VPL iliisha kwa sare ya bao moja na kushuhudiwa kandanda safi la kushambuliana likitandazwa.

Mchezo wa mapema utakaopigwa leo ni ule utakaowakutanisha Simba na Chipukizi mishale ya saa 10:15 jioni ambapo utakuwa ni mchezo wa kwanza msimuu huu kwa Simba kucheza bila ya aliyekuwa kocha wake mkuu mbelgiji Sven Vanderbroeck ambaye jana imethibitika kuachana kwa makubaliano.

Kocha msaidizi wa Simba wa sasa Selemani Matola ndiye anayekaimu nafasi hiyo mpaka pale wekundu wa msimbazi hao watakapomtangaza kocha mpya atakayewanoa na kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya michuano mikubwa ya klabu bingwa barani Afrika.