Yaliyotokea usiku wa UEFA

Wednesday , 13th Sep , 2017

Msimu wa UEFA 2017/18 umeanza rasmi usiku wa kuamkia leo kwa michezo nane kupigwa huku mambo mbalimbali yakijitokeza zikiwemo rekodi kwa baadhi ya timu pamoja na wachezaji.

Nyota wa Barcelona Lionel Messi kwa mara ya kwanza amefanikiwa kumfunga golikipa wa Juventus Gianluigi Buffon baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa Barcelona wa mabao 3-0. Katika mchezo huo Buffon ametimiza michezo 117 ya UEFA.

Manchester United walikuwa wanarejea kwenye michuano hiyo baada ya kuikosa msimu uliopita na mshambuliaji wake mpya Romelo Lukaku ameingia kwenye orodha ya wachezaji waliofunga katika mchezo wao wa kwanza wa UEFA baada ya kupachika bao moja dhidi ya FC Basel.

Muunganiko wa washambuliaji wa PSG Mbappe, Cavan na Neymar wanaounda 'MCN' wameendelea kufumania nyavu kwa pamoja baada ya kuilaza Celtic 5-0 huku Kylian Mbappe akiweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufikisha mabao 7 katika michuano hiyo.

Chelsea kwa mara ya kwanza imefunga mabao 6 chini ya kocha Antonio Conte baada ya kuifunga Qarabag mabao 6-0. Bayern Munchen wameweka rwekodi ya kushinda michezo 14 mfululizo ya ufunguzi wa hatua ya makundi.