Jumamosi , 24th Jun , 2017

Mchezaji wa Kimataifa wa kutoka Kenya anayechezea klabu ya Tottenham Hotspurs, ya ligi kuu ya soka nchini Englad, Victor Wanyama, amesema endapo Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ataongeza bidii anaweza kwenda kuchezea Ligi Kuu ya Uingereza.

Mchezaji Victor Wanyama

Wanyama ameeleza hayo kupitia kipindi cha FNL kutoka EATV usiku wa kuamkia leo na kusema Samatta ameweza kufungua njia kwa wachezaji wa Tanzania na endapo ataendelea kufanya vizuri basi atakuwa amejiweka katika nafasi nzuri ya kuzidi kucheza mpira kimataifa zaidi.

"Samatta amefungua njia kwa hapa Tanzania kwa hiyo wachezaji wengine wakipata nafasi wasikate tamaa, msimu huu Samatta amefanya vizuri sana na kama ataendelea kufanya vizuri katika msimu ujao basi atakuwa na nafasi ya kucheza Ligi kuu ya Uingereza. Anachotakiwa kufanya ni kutia tu bidii zaidi" alisema Wanyama.

                                                            Mchezaji Mbwana Samatta

Pamoja na hayo, Wanyama amewataka wachezaji wa Tanzania na Afrika Mashariki kiujumla kuacha kukata tamaa mapema kwa kile wanachokihaingaikia katika masuala mazima ya mpira.

"Wachezaji wa huku tunakata tamaa mapema na kuridhika haraka, kama mchezaji ukitaka kufanikiwa unatakiwa ku-focus katika mpira tu, usichanganye na mambo mengine" alisisitiza Wanyama.