Ijumaa , 8th Jan , 2021

Licha ya kuipongeza klabu ya soka ya Simba kutinga hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, mshauri wa michezo nchini Dokta Jonas Tiboroha amewataka wawakilishi hao wa nchi kufanya usajili katika idara ya ulinzi na kiungo ili kuimarisha kikosi chao.

Mshauri wa michezo nchini, Dokta Jonas Tiboroha (Kushoto) pichani enzi zake akiwa kiongozi katika klabu ya Yanga.

Dokta Tiboroha ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Klabu ya Yanga amesema hakuwahi kuwa na mashaka na nafasi ya Simba kutinga hatua ya makundi msimu huu, kwakuwa aliona kikosi chao kilikuwa na nguvu zaidi kuliko wapinzani waliokutana nao.

''Kitu ninachowashauri Simba ni kuongeza nguvu katika idara yao ya ulinzi, wanao wachezaji wazuri lakini umri wao ni mkubwa hilo lipo wazi, hawatoweza kuhimili kasi ya washambuliaji wa timu zenye ubora wa haliya juu na hilo linajulikana.

Vilevile ninaona wanahitaji kuongeza kiungo katika idara ya kiungo, wamemsajili Thadeo Lwanga lakini bado sijamuona, ila ukweli ni kwamba kwaninachokiona hawa waliopo hawatoshi kuwavusha Simba, labda itategemea na kundi watakalopangwa'' alisema Dokta Tiboroha.

Kuhusu tofauti ya ubora kati ya kikosi cha msimu huu na cha msimu juzi ambao Simba walitinga robo fainali ya michuano ya CAF, Dokta Jonas Tiboroha amesema kikosi kilichokuwa kikinolewa na Patrick Aussems kilikua bora zaidi kwakuwa wachezaji nao walikuwa katika kiwango chao, lakini hiki kilichokuwa kikifundishwa na Sven Vandenbroeck kinacheza kwa mbinu nzuri za mwalimu na wanacheza kitimu zaidi.

''Simba ya Aussems ilikuwa na wachezaji bora sana, Meddie Kagere wa kipindi kile sio wa sasa, hata Jonas Mkude, na Erasto Nyoni nguvu imepungua bali wana uzoefu, walikuwa na mtu mwenye kasi kubwa Emmanuel Okwi, wapo wakina Luis Miquissone na Clatous Chama wanauwezo mkubwa lakini nikilinganisha na Simba ile naona kunasehemu inawazidi'' Jonas Tiboroha.

Hata hivyo Tiboroha amedai kwamba iwapo Simba itazingatia kwa kufanya usajili mkubwa katika idara alizopendekeza, ipo siku watu watakimbiana uwanjani kwakuwa wana timu bora sana.