Jumanne , 23rd Mei , 2017

Timu ya soka ya wanawake 'Twiga Stars' imeanza maandalizi na mchujo wa kupata wachezaji watakaoweza kuungana na kikosi cha timu ya wakubwa kwaajili ya kujiandaa kufuzu michuano ya AFCON inayotarajiwa kutimua vumbi mwakani nchini Ghana.

Wachezaji wa Twiga Stars wakiwa katika mazoezi

Hayo yamebainishwa na Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Edna Lema ambaye amesema kwamba baada ya kuanza kambi rasmi watajitahidi kucheza michezo ya kujipima ubavu na timu zenye uwezo kisoka ikiwemo nchi za Nigeria, Ivory Coast pamoja na Ghana.

"Tumeita wachezaji 45 na baada ya wiki moja tutachuja wachezaji tutabakiwa na wachezaji 25 mpaka 30 ambao katika timu hiyo hiyo tutakuwa na wachezaji watakaocheza U-20 na wengine watacheza ile timu ya wakubwa...Tuna programu ya kucheza mechi za kirafiki lakini siyo kwa mazoezi tunayoyafanya kwa sasa". Alisema Edna

Kocha huyo aliendelea kwa kusema "Mazoezi tunayoyafanya kwa sasa  ni kwa sababu sasa hivi kikubwa tunachoangalia ni kufanya mchujo kwa ajili ya kupata wachezaji watakaotusaidia baadaye, baada ya hapa kambi itakayofuata tutaomba mechi mbili au tatu tuweze kuona ni wachezaji wa aina gani ambao tumewapata na ambao tunao ili waweze kutusaidia katika kampeni zetu za kwenda kucheza AFCON mwakani nchini Ghana,"