Tumeifunga Atletico kwa ushawishi- Tuchel

Jumatano , 24th Feb , 2021

Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel amewapongeza wachezaji wake kwa ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Atletico Madrid ya Hispania jana usiku, kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Olivier Giroud akifunga bao

Mchezo huo ulichezwa Bucharest nchini Romania na sio Hispania kutokana na masharti magumu ya kujikinga na maambukizi ya Covid -19 yaliyopo nchi humu kutoka kwa wageni nchini England.

Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Olivier Giroud dakika ya 68, baada ya mchezo huo kumalizika kocha Tuchel alionyeshwa kuridhishwa na ubora wa timu kwa ujumla

''Nimefurahi sana kwa kiwango walichoonyesha wachezaji wangu tumepata matokeo makubwa na yanaonekana kwenye ubao wa matokeo, kwamba tumepata matokeo mazuri kwa kiwango bora. Ilikuwa muhimu sana kwasababu tulitawala mchezo kwa dakika zote 96 na tunakubali ilikuwa ngumu sana kutengeneza nafasi lakini ilikuwa juhudi nzuri sana ya timu.''

Kwa upande mwingine Kocha huyo mjerumani akamwagia sifa mfungaji wa bao hilo la pekee katika mchezo huo Olivier Giroud.

''Ukimwona kila siku huwezi kushangaa. Yuko sawa kabisa, mwili wake uko sawa, umbo lake liko kwenye kiwango cha juu na kiakili, nina hisia anayafurahia kila siku, hiki ndicho kiwango anachohitaji kuwa nacho. Anafanya mazoezi kama mtoto wa miaka 20.

Huu ni ushindi wa 6 tangu kocha Thomas Tuchel aanze kukinoa kikosi cha the Blues katika michezo 8. Mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Atletico Madrid utachezwa nchini England katika dimba la Stanford Bridge Machi 17, 2021.