Jumatano , 27th Jan , 2021

Kocha mpya wa Chelsea, mjerumani Thomas Tuchel atakiongoza kikosi hicho kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Wolves, mchezo wa ligi kuu England katika dimba la Stanford Bridge.

Kocha mpya wa Chelsea, mjerumani Thomas Tuchel

Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 47, alitangazwa rasmi jana usiku kuwa kocha mpya wa 'The blues' kwa mkataba wa miezi 18, akichukua mikoba iliyoachwa na kocha Frank Lampard aliyefutwa kazi siku ya Jumatatu na mmiliki wa timu hiyo bilionea wa kirusi Roman Abromovich, kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo. 

Kibarua cha kwanza cha Tuchel ni kuhakikisha Chelsea inapata matokeo mazuri kwenye michezo yake, kipimo cha kwanza ni kuanzia mchezo wa usiku wa leo dhidi ya Wolves. Mwenendo wa kikosi hicho haujawa mzuri katika michezo 8 ya mwisho ya EPL, Chelsea imeshinda michezo 2 wakifungwa michezo 5 na wametoka sare mchezo 1. Kikosi hicho kipo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa EPL kikiwa na alama 29.

Mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Wolves, Chelsea walifungwa mbao 2-1 katika dimba la Molineux. Mchezaji pekee ambaye anaweza kukosekana kwenye kikosi cha Tuchel ni Ngolo Kante, wengine wote wapo fiti kucheza.

Tuchel anakuwa kocha wa kwanza mjerumani kuifundisha Chelsea na anakuwa kocha wa 13 anaajiriwa chini ya utawala wa Roman, ukiachana na makocha ambao walipewa mikataba ya muda mfupi.