Tuchel amwagia sifa Olivier Giroud

Jumatano , 24th Feb , 2021

Kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel amemwagia sifa mshambuliaji wake Olivier Giroud baada ya nyota huyo kufunga bao moja na la ushindi dhidi ya timu ngumu ya Atletico Madrid kwenye mchezo wa mtoano mkondo wa kwanza hatua ya 16 bora klabu bingwa barani Ulaya uliochezwa usiku wa jana.

Kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel akimpongeza mshambuliaje wake Olivier Giroud baada ya kufunga bao na kumfanyia mabadiliko usiku wa jana.

Tuchel amesema “Ukimuona kwenye mazoezi ya kila siku, huwezi kushangazwa na alichokifanya. Mwili wake upo kwenye utayari na utimamu wa hali ya juu. Anafanya mazoezi kama kijana wa miaka 20 au 24”.

“Ni mtu mwenye umakini sana na utani awapo mazoezini. Muda wote ana mawazo chanya jambo ambalo ni muhimu sana kwenye timu. Akianza au akitokea benchi bado ana ubora kitu ambacho ni kizuri”.

Olivier Giroud mwenye umri wa miaka 34, alifunga bao hilo dakika ya 68 kwa 'Tik taka' na kuwashangaza wengi kutokana na uzuri wa bao hilo na kuifanya timu yake kupata ushindi na faida ya bao 1-0 ugenini kwenye mchezo ulichezwa Bucahrest nchini Romania.

Olivier Giroud akiifungia bao timu yake ya Chelsea usiku wa jana dhid ya Atletico Madrid.

Bao hilo ni la 6 kwa Giroud kwenye michuano hiyo msimu huu ikiwa ni mengi zaidi kwenye msimu mmoja tokea kucheza michuano hiyo, lakini akifikisha mabao 11 katika michezo 22 katika michuano yote msimu huu akiwa na Chelsea.

Kwa upande wa kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone amekiri ubora wa Chelsea kwenye mashambulizi na kusema imewalazimu kucheza kwa kujilinda zaidi jambo hata lililopelekea kucheza bila kupiga shuti hata moja lililolenga lango tokea wafanya hivyo mara mwaka 2017 dhidi ya Juventus.

“Ilikuwa ni mechi ngumu, hakuna timu iliyopata nafasi nyingi za kufunga. Lakini pia ilikuwa ngumu kutokana na ushambuliaji wao kwasababu wanawachezaji wenye nguvu na ubora”.

Kipigo hiko kinaifanya Atletico Madrid kusalia na ushindi mmoja tu katika michezo yake 5 ya mwisho, akifungwa mchezo wa pili mfululizo na kutoa sare mbili.

Wawili hao wanataraji kurudiana mapema mwezi ujao kwenye dimba la Stamford bridge jijini London nchini England.