Alhamisi , 2nd Jun , 2016

Wakati timu ya taifa ya mchezo wa Tenisi kwa walemavu ya Tanzania ikijiandaa na michuano ya wazi ya Kenya timu hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa fedha kwaajili ya maandalizi na pia vifaa hasa viti vya magurudumu ambavyo ndiyo kama miguu yao.

Wachezaji wa timu ya tenisi ya walemavu ya Tanzania wakipeana mikono baada ya mchezo wao.

Kocha Mkuu wa kikosi cha timu ya taifa ya Tenisi ya walemavu ya Tanzania [Wheel chair tennis] Riziki Salum anawaomba wadau kuisaidia timu hiyo ambayo iko katika maandalizi ya kushiriki michuano ya kimataifa katika ya mwezi huu.

Timu hiyo inataraji kushiriki michuano ya kimataifa ya wazi ya Kenya [maarufu kama Kenya Open] inayotaraji kufanyika kuanzia Juni 18 mwaka huu jijini Nairobi nakushirikisha mataifa kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Riziki amesema timu hiyo ni kinara wa mchezo huo kwa nchi za Afrika Mashariki na kati na inataraji kushiriki pia michuano ya Olimpiki ya Rio Brazil itakayofanyika mwezi Agasti mwaka huu.

Riziki amesema pamoja na mafanikio hayo yote ikiwemo ya kushika nafasi ya pili kwa bara la Afrika lakini timu hiyo imekosa udhamini kitu ambacho kinapelekea kutofanya vizuri zaidi katika michuano mikubwa ya kimataifa hasa ya dunia kutokana na kukosa maandalizi ya kutosha.

Aidha Riziki amesema pamoja na sapoti kidogo kutoka kwa baadhi ya Wadau hasa kutoka klabu ya Gymkhana bado timu hiyo inahitaji kuungwa mkono na Watanzania wote, makampuni na Serikali ili iweze kufanya maandalizi yenye tija na kuweza kuiletea sifa nchi katika medani ya kimataifa.

kocha huyo amesema wachezaji wa timu hiyo wanauwezo mkubwa ila kinachowakwamisha ni udhamini wa masuala mbalimbali muhimu na pia changamoto kubwa ni vifaa hasa viti vya magurudumu [wheel chairs] ambavyo ndiyo kama miguu yao ya kutembelea wakati wa mchezo.