Tanzania dhidi ya DR Congo LIVE East Africa Radio

Jumanne , 12th Jan , 2021

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars' inataraji kushuka dimbani saa 11:00 jioni ya leo tarehe 12 Januari 2021 kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya DR Congo mchezo utakaochezwa kwenye dimba la mkapa jijini Dar es salaa na kutangazwa mubashara na EA radio.

Mchezo huo ni wa maandalizi kwa Stars ambayo alfajiri ya tarehe 14 Januari 2021 inatazamiwa kusafiri kuelekea nchini Cameroon kushiriki michuano ya wachezaji wa bara la Afrika wanaocheza ligi za ndani CHAN inayotaraji kuanza tarehe 16 Januari 2021.

Kuelekea kwenye mchezo huo kocha msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda amesema “yale ambayo tumewaelekeza wachezaji, yale ambayo tutaenda kuyafanya Cameroon ndiyo tutayafanya kesho ili tujue wapi pakuongeza wapi pakupunguza”.

Mchezaji mpya wa kikosi cha Yanga, mlinzi wa kati Dickson Job atakosekana kwenye mchezo huo kutokana na kuendelea kuuguza majeraha yake ya mguu. Kocha Mgunda amesema kabla kikosi hicho hakijaondoka na kwenda Cameroon watatangaza kikosi kamili kitakachoshiriki CHAN 2021.

Nae mchezaji mkongwe kikosini, mlinda mlango Juma Kaseja amesema “Maandalizi yameenda vizuri na tunaendelea kujiandaa naamini mchezo wa kesho wa kirafiki utawapa nafasi walimu kuangalia  mapungufu ya mchezo wa kesho na kuyafanyia kazi wakati tunaenda kwenye tournament”.

Mchezo utakuwa ni wa tatu kwa Taifa Stars kukutana na DR Congo kwenye michezo ya kirafiki ya kimataifa na Stars akiwa na rekodi nzuri ya kupata ushindi kwenye michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja.

Mchezo huo ambao utachezeshwa na mwamuzi wa kati Ramadhani Kayoko kutoka Dar es salaam, utakuwa na tukio maalum la kumuaga mchezaji wa muda mrefu kwenye kikosi cha timu ya taifa mlinzi wa kati Aggrey Moris ambaye atatangaza rasmi kutundika daruka kwenye timu ya taifa Taifa Stars.

Kituo chako bora cha matangazo cha East Africa Radio na watangazaji wake bora wa michezo Abissay Stephen JR na Mwalimu Lukinja Tigana wanakutangazia mchezo huo mubashara kutoka dimba la mkapa saa 11:00 jioni ilhali George Kampista na Mtaalam Ibrahim Kasuga watakuletea uchambuzi kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10:30 jioni. Ishu ni kusikiliza EA radio.