Alhamisi , 31st Mar , 2016

Baadaya ya kilio cha muda mrefu cha wanamichezo mbalimbali hasa wa soka nchini Tanzania wa maeneo ya vijijini hatimaye kilio chao kimesikika na kupata jibu hii leo baada ya klabu ya Sunderland kusaini mkataba wa kukuza soka vijijini kanda ya ziwa.

Wawakilishi wa Sunderland AFC, TFF na ACACIA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini mkataba wa kukuza soka nchini.

Klabu maarufu ya soka nchini Uingereza ya Sunderland AFC ambayo inashiriki ligi kuu ya soka ya Uingereza ijulikanayo kama Barclays Premier Ligi, hii leo imeingia mkataba na Kampuni ya ACACIA kwa kushirikiana na TFF wenye lengo la kuendeleza soka hapa nchini kuanzia ngazi ya chini hasa vijijini kule kanda ya ziwa.

Mara baada ya kusaini mkataba huo wa miaka miwili wenye thamani ya kiasi cha pauni laki moja na nusu za Uingereza wawakilishi wa Sunderland, ACACIA na TFF walizungumzia machache kuhusu ushirikiano huo ambapo wamesema ni mkataba wenye lengo mama la kuibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi katika lengo la kupata timu bora za wakubwa za baadae ambazo zitatutangaza imataifa katika michuano mbalimbali.

Sunderland pia imekywa na ushirikiano mzuri na makampuni mengine hapa nchini ushirikiano ambao ni mkakati wa klabu hiyo kuimarisha uhusiano na taasisi mbalimbali zilizopo barani Afrika na wenye lengo la kunufaisha jamii inayozunguka taasisi hiyo ikiwemo katika kuendeleza sekta ya michezo hasa kwa vijana wadogo nchini.

Na katika kuhakikisha ama kufanikisha mchakato huo Mkuu wa kitengo cha kuendeleza mchezo wa soka kimataia wa klabu ya Sunderland Graham Robinson ameshatembelea na kufahamu maeneo ambayo yamelengwa kunufaika na mradi huo ambapo tayari klabu za wilaya za Tarime na Kahama zitaanza kupata mafunzo hayo kwa makocha na vijana ambapo klabu ya Sunderland itatenga wiki 10 kwa mwaka kufanya kazi na klabu hixo katika lengo la kukuza mpira wa miguu nchini.

Mwisho wadau hao wamesema ni vema kwa wahusika kuulea na kuuheshimu ushirikiano huo kwani utakuwa na faida kubwa kwao na kwa jamii nzima na taifa kwa ujumla kwani kwakuwa ushirikiano huo utalenga katika kukuza na kuinua vipaji vya mchezo wa soka lakini pia timu hiyo kupitia wataalamu wake waliobobea katika mafunzo ya ualimu na vijana watawapatia vijana wazawa toka kanda ya ziwa maeneo hayo yaliyozunguka migodi ya Acacia mafunzo ama ujuzi wa kufundisha soka ambao watautumia kufundisha vilabu vidogo vidogo vilivyopo kwenye maeneo ya jamii hizo na hivyo kuleta mabadiliko makubwa katika soka la vijana wadogo kwa jinsia zote.