Alhamisi , 29th Sep , 2022

Winga wa Tottenham Hotspur Lucas Moura amesema msimu huu kikosi chao kina nafasi kubwa zaidi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England EPL. Na anaamini ubora wa kikosi na kocha Antonio Conte ni miongoni mwa sababu zinazomfanya aamini watakuwa mabingwa.

Lucas Moura (upande wa kulia) huu ni msimu wake wa 6 yupo na kikosi cha Spurs

Huu ni msimu wa 6 kwa Moura akiwa na kikosi cha Tottenham, alijiunga na timu hiyo mwaka 2017 akitokea PSG ya Ufaransa, winga huyo raia wa Brazili amesema ubora wa kocha, wachezaji na timu kwa ujumla ni sababu zinazomfanya aone kikosi hicho kina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.

"Kusema kweli, kati ya misimu yote ambayo nimekuwa hapa, nadhani huu ndio msimu ambao tuna nafasi nzuri zaidi, matarajio yetu ni makubwa zaidi. Nadhani tunaweza kuwania taji kwa sababu ya ubora wa kikosi, ubora wa kocha na timu kwa ujumla. Kikosi kimeimarika katika miaka hii na kimekuwa kikiimarika zaidi katika ngazi ya taifa na dunia. Tottenham ya leo ina nguvu kubwa katika soka. Ninaamini kwamba kwa miaka yote ambayo nimekuwa hapa, huu ndio mwaka ambao tunaukaribia zaidi ubingwa.’’ Amesema Lucas Moura

Spurs wameanza msimu huu wa 2022-23 vizuri hawajapoteza mchezo hata mmoja kwenye michezo 7 ya awali waliyocheza mpaka sasa na wamekusanya alama 17 wapo nafasi ya 3 wakiwa na alama sawa na Manchester City wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ikiwa ni tofauti ya alama 1 dhidi ya vinara Arsenal wenye alama 18.