Solskjaer awatupia lawama waamuzi

Jumatatu , 1st Mar , 2021

Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amemtupia lawama mwamuzi wa kati, Stuart Atwell kwa kushindwa kutoa penalty kwa upande wao baada ya kudai winga wa Chelsea, Callum Hudson-Odoi aliucheza mpira kwa mkono jambo lilipelekea wakose ushindi muhimu.

Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer.

Solsjkaer amesema, licha ya tukio kutazamwa zaidi ya mara moja na jopo la waamuzi wa VAR lakini hakuweza kupata penalti hiyo na kuamini sababu iliyopelekea wadondoshe alama mbili ni maamuzi mabovu ya mwamuzi huyo wa kati na jopo zima la VAR.

Kwa upande wa kocha wa Chelsea, Thomas Tuchel amekiri kuwa na mtazamo tofauti na kocha wa Manchester United, Solskjaer na kuamini tukio hilo halikuwa penalti na kushangazwa kwanini ililazimika jopo la waamuzi wa VAR kurejea tukio hilo.

Baada ya sare hiyo, Manchester United imesalia nafasi ya pili ikiwa na alama 50 utofauti wa alama 12 na kinara Manchester City mwenye alama 62 wakiwa na idadi sawa ya michezo, michezo 26 ilhali Chelsea imekwama kwenye nafasi ya tano ikiwa na alama 44.