Jumanne , 21st Feb , 2017

Kuelekea katika mpambano wa watani wa jadi Simba na Yanga, viongozi wa matawi mbalimbali ya vilabu hivyo wameendelea kutambiana huku wakiitaka serikali kumchukulia hatua mtu yeyote atakayegundulika kufanya uharibifu katika mchezo huo.

Mashabiki wa Simba na Yanga Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam

Mwenyekiti wa tawi la Mpira Pesa kwa upande wa Simba Ostadh Masoud amesema, mechi zote wanazokutana na Yanga wanaziheshimu na kikosi cha Simba kimejipanga vizuri na kwa umakini ili kuweza kuibuka na ushindi kwani lengo lao hasa ni ubingwa ili kuweza kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.

"Lazima tuongeze umakini kwasababu Yanga tulimkimbia kwa pointi nane leo hii ametukuta tunatofautiana kati ya pointi moja au mbili kwa hiyo anaonekana kuna kitu anakitaka kwa maana hiyo lazima niwaambie wana Simba hata wachezaji kwa ujumla hii ni fainali na kila mtu ambaye anaamini ana kitu ambacho kitasaidia Simba ishinde kitumike, " amesema.

Kuhusu vurugu, Ostadh amesema "Mimi niwaambie tuu mashabiki kuwa watulivu katika mchezo wa Februari 25, Mwamuzi akishapuliza kipyenga hakuna wa kupinga hata ukienda mahakama kuu, sisi tujikite kuhakikisha timu yetu inashinda na tusitegee kushindwa au sare, " amesema.

Kwaupande wake Katibu wa tawi Yanga la Tandale kwa Mtogole Waziri Jitu amesema, wanaamini wataibuka na ushindi katika mchezo huo kwani kikosi chake ni bora na Simba wasitegemee kama wataweza kubeba pointi tatu katika mchezo huo.

"Sisi tunajiamini na kazi tumeshamaliza tusubiri tuu siku ya jumamosi tufike Uwanjani kuhitimisha, mimi nina timu bora kwani Afrika Mashariki hii ikiangalia timu bora ya kwanza Yanga na inafuatiwa na Azam FC kidogo, " amesema.