Jumatano , 22nd Feb , 2017

Tambo zimeendelea kuvuma kuelekea mpambano wa watani wa jadi Simba na Yanga siku ya Jumamosi, ambapo leo hii Mjumbe wa kamati ya mashindano ya Yanga SC , Salum Mkemi amesema siku hiyo Simba hawachomoki, na ni lazima wafungwe.

Salum Mkemi

Mkemi amefunguka na kusema kuwa hakuna namna nyingine zaidi ya timu yake hiyo kuibuka na ushindi mnono dhidi ya Simba kwenye mchezo huo wa ligi kuu bara ambao ni wa marudiano baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dare es Salaam, Salum Mkemi amesema Yanga wamejipanga vyema kila idara na kudai watazidi kuongeza idadi ya makombe kila mwaka kwa kuibuka na ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

"Tumejipanda kikamilifu kila idara kuhakikisha tunaibuka na ushindi siku ya Jumamosi mbele ya watani wetu wa jadi Simba SC, haya ni makombe yetu na tutazidi yaongeza kila mwaka hivyo hakuna njia nyingine kwetu kuelekea mchezo wetu huo zaidi ya ushindi tu," alisema Salum Mkemi

Aidha Bw. Mkemi aliendela kusema kipigo watakachokipata Simba si cha kawaida na ndiyo itakuwa mwisho wa timu hiyo kushiriki mashindano hayo kwakuwa itashushwa daraja.

Hata hivyo Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF), limewatahadharisha mashabiki kuacha kuingia na mabango yenye uchochezi wa aina yeyote au kumtaja kiongozi wa serikalini.